Ni kweli, lazima tutangulize siha ya moyo kabla ya silaha. Na silaha ya kwanza katika vita yoyote ile ni mawasiliano sawia. Sakramenti ya lugha ni muhimu sana. Lugha za kuagiza, za jumla-jumla na kauli za imla, badala ya kusaidia, huchanganya watu zaidi.

Kwa mfano, Kiranja Mkuu anasema tujifukize mitishamba, mwingine anasema hiyo ni hatari kwa afya, na wengine tumeze klorokwini. Miluzi mingi, kama walivyonena wahenga, humpoteza mbwa. Hakika, hii korona imetufumania na itatufunulia mengi!

Nasisitiza hivi, kwa sababu yamenikuta njia panda, baada ya mlipuko wa hii korona ilibidi nipige simu kwetu kijijini, hasa ndugu yangu Kunawa bin Barakoa. Kabla ya kuwapa taarifa na tahadhari za korona na haja zake, ilibidi niwashirikishe badala ya kuwasemea namna ya kujikinga na huu ugonjwa. Hili ni muhimu sana. Natubu, haikuwa rahisi maana kuna vitendo na fikra ambazo hazina tafsiri katika lugha zetu mama.

Ima fa ima, korona inatukoroga wengi. Kuna wakati unakaa umelowa karantini kama umelogwa hivi. Kuna vitu vitatu ambavyo kihistoria vimebadilisha sana dunia: Magonjwa, Mapinduzi na Vita. Na kuna vita tayari vya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambavyo hii korona imeamsha.

Rais wangu hapa Brazil, Jair Messias Bolsonaro, anahisi kama anataka kupinduliwa. Amekosa umaarufu. Anafanya rafu. Amejificha kipindi ambacho anahitajika zaidi. Alifikiri uraisi ni kuongoza mitala au kabila fulani.

Urais sio ulaji ni uwajibikaji. Kuna kila dalili na harufu ya kurudi miaka ya 1964 ya udikteta. Siteti wala kutetea. Hii korona inatuonesha aina ya viongozi tulionao.

Turudi nyumbani…

Basi nikaeleza na kujieleza kuwa korona imetoka nje. Sio zao letu, ila ni zali letu sote. Sisi ni rika la waathirika zaidi. Baadhi ya tahadhari, kwao zilikuwa ni athari zaidi; eti wakae ndani, wamwite daktari wakizidiwa, wanawe mikono na uso mara nyingi, watumie kitakasa na barakoa.

Kwanza, walinicheka mpaka kamasi ziliwatoka, kwa maana hivi ni vitu ambavyo ni gharama zaidi kuliko matumizi yao ya kawaida. Kwa hiyo, hatukuongea lugha moja. Walisema naongea kitamko sana.

Lengo la hii vita ni kujiongezea umiliki mali na himaya kama kawaida, nilifikiri fikirika. Kumbe nilifilisika na nilikosea sana. Sasa naona mshindi wa hii vita ni taifa lililowekeza na litakalowekeza zaidi katika sayansi, uongozi madhubuti, miundombinu ya afya na elimu kwa ujumla.

Na zaidi, mshindi ni jamii itakayozalisha tunu za uaminifu, ushirikiano na utumishi bora. Tuanze kwa kunawa mikono, kujiokoa na viongozi aina ya watemi kama Donald Trump na Jair Messias Bolsonaro waliojaa Afrika pia. Ingetokea sasa, dili la kunywa kikombe cha Babu wa Loliondo litokee, hawa watemi wangekuwa wa kwanza kunywa.

Huyu adui nduli hana mazingara wala mizinga. Ila yupo amezagaa kama dagaa. Korona inakuja kwa kasi na sarakasi hadi kupindua thamani ya vitu; tazama, petroli bila walaji imetuwama tu, ardhi imefurahi maana sasa inapumua. Kabla ya korona kuvaa barakoa kulifananishwa na ugaidi fulani, lakini sasa ni sheria lazima uvae.

Katika lugha zote neno ambalo limesikika zaidi kipindi hiki ni nyumba. Kaulimbiu za-#StayHome, #BakiNyumbani, #FiqueEmCasa, zinapishana mbio mitandaoni maana ndio dawa kwa sasa. Lakini pia talaka, unyanyasaji na ukatili dhidi ya wazee na watoto umeongezeka. Sambamba na hayo, ni kama tulihitaji hivi virusi kujua tofauti kati ya nyumba na nyumbani. Bila visigino, hatuna visingizio vya kuchelewa kurudi nyumbani.

Tulihitaji hii korona kutambua wajibu na nafasi ya elimu majumbani. Kumbe shule ina wajibu wa kufundisha na jukumu la familia ni kuelimisha. Umeelewa tofauti? Na eti hivi, kipaumbele kwetu, ni elimu au siasa za elimu? Na falsafa yetu ya elimu ni ipi?

Na kuhusu, kufundisha kupitia luninga na mitandao, isingekuwa hili janga la korona, labda ingetubidi kutunga kufanya muswaada bungeni, jambo ambalo lingechukua muda na labda tusingefanikiwa. Asante korona kwa kurahisisha mambo. Sasa tunajua kwamba kufundisha sio rahisi na walimu (napendelea kuwaita wakunga na wauguzi) ndio mashujaa kuliko wanasiasa.

Halafu, sijasikia wanasiasa wakijinyima posho zao ili zisaidie hii vita. Au wanataka mpaka kupigiwa magoti? Katika maongezi kule nyumbani niliona aibu kuwadanganya, eti hii korona imetusawazisha wote, kwamba hakuna tofauti kati ya matajiri na maskini.

Hata kama dunia nzima imejikuta katika chungu kimoja, bado uchungu wake ni tofauti. Ili tu uweze kukaa ndani karantini inamaanisha kuwa na akiba ya chakula, kumudu vitakasa na watoto kusomea nyumbani ni anasa au upendeleo fulani. Kusema tubaki nyumbani, ni lugha ya jumla sana na isiyoeleweka kwa wengi. Hapa ndipo tunahitaji weledi wa viongozi, kutegua hiki kitendawili.

Kimsingi, hii korona imefukua makaburi na kiburi cha huu mfumo duni wa kiliberali ambao tuliudandia kwa nyuma. Tunasindikiza na uhai wetu ukisindikwa. Nategemea Raisi na wabunge kipindi hiki wapunguze ushuru kwenye bei ya bidhaa muhimu kabla ya kuomba kufutiwa madeni na mashirika ya fedha duniani. Natafakari na kujikuna maisha (mbadala) baada ya korona yatakuwaje?

Je, Tanzania mpya itazaliwa baada ya tanzia hii? Tushirikishane. Kuna kitu tumejifunza (utayari wetu kwenye majanga, tumeona aina ya viongozi na mfumo wa kiutawala tulionao, na mfumo wetu wa afya) au tutarudi na bendera ile ile ya bora liende? Kwa bahati mbaya, mambo ya ubuyu, maslahi binafsi, uchama zaidi na kubeti/mkeka ndio yanayoonekana kuongoza nchini kuliko mambo ya msingi.

Kwa maneno mengine, wengi wetu ni sehemu ya tatizo. Tusiwe kama yule mpumbavu ambaye wakati nyumba yake inateketea alijikita kuwashughulikia panya waliokuwa wanakimbia moto. Ndivyo alivyosimulia gwiji wa fasihi Chinua Achebe alipokuwa akielezea uzembe wetu.

Tazama nipo hapa mimi na mwili wangu nategemea sana ushirikiano kati ya vidole na ubongo ili kuendelea kuandika. Sasa nahisi upweke na nimegawanyika. Roho ipo nyumbani lakini mwili upo ugenini. #BakiNyumbani.

Twita @Isaac29g

--

--