YA MTANDAONI NA MTANDIONI

@IsaacGaitano
4 min readAug 16, 2020

Kitu ambacho kizazi hiki kinahitaji kufundwa zaidi ni NIDHAMU katika kila kitu, iwe ya kazi, muda, mahusiano na pia USTAHIMILIVU ambao sio sawa na uvumilivu.

Katika nyakati nyeti za uwazi na utandawazi, maisha bila mtandao hayawezekani. Huduma za internet sio starehe tena, zimekuwa ni haki na wajibu wa kiraia. Iwe taasisi, kazi au biashara zake zozote zile, zinahitaji mtandao fulani ili kujiimarisha na kuendelea kuwepo duniani. Ni ukweli kwamba, mabadiliko yaletwayo na utandawazi, yanakuja kwa kasi ya hali ya juu na ni makubwa kuliko uwezo wetu wa kuyahimili. Leo watu wanasema sio kabla ya Kristu na baada ya Kristu bali kabla ya google na baada (mbadala) ya google. Changamoto na faida ni nyingi katika karne hii ya Habari na Teknologia. Ndugu mpenzi msomaji, leo nataka tuongelea kuhusu teknolojia na afya hasa ya akili.

Tunakua na kushinda kwenye (na) dunia ya mitandao mbalimbali, (huu ni uhalisia sio nadharia tena) kama Facebook, Instagram, whats up, nk. Naam, ya mtandaoni ni mengi, kama wasemavyo walimwengu. Kama vile mitandio kwa akina mama, mitandao imekuwa kama kitambulisho chetu kipya cha uwepo wetu duniani. Mtu yupo tayari kukosa pesa ya kununua chakula, lakini sio pesa ya vocha ili kujiunga na mitandao. Lakini, uhalisia wa maisha ni tofauti na yanayoonekana na kuoneshwa mitandaoni (virtual versus real life).

Mtandaoni kila mtu anaonekana meno nje, ameyapatia maisha, ametoka na kutoboa kweli kweli. Hali zetu duni tunazionea aibu, hivyo tunazificha uvunguni. Hii mbinu haisaidii, ni butu. Tunajenga kizazi kinachokosa kujiamini, bali legelege, kinashindwa to face the real life challenges. Kizazi kinajianika masaa 24 mwambaoni mwa mitandao. Wataalamu wanasema, unapotumia simu na mitandao ya kijamii, ubongo wetu hutoa kemikali inayoitwa Dopamine, ndio maana unapopokea ujumbe fulani unajisikia vizuri. Mtu anaamka asubuhi, cha kwanza, bila hata sala ya shukrani, ni kuangalia na kusalimia wafuasi wake mtandaoni, kabla ya ndugu zake hapo jirani.

Hii kemikali ya Dopamine (wananeurosciencia wanaelewa vizuri zaidi) ndio inakufanya ujisikie raha unapovuta sigara, bangi, unapocheza upatu au kunywa pombe. Kumbe, hii kemikali ina uraibu (addiction) mkubwa.

Tukiwa wadogo tunahitaji kukubalika na kupendwa na wazazi, walezi wetu. Bila shaka, ni haki yetu. Kijana anapoingia kubalehe,anahitaji kukubalika na kundi la rika lake zaidi kuliko wazazi wake. Hapo unaanza kuwategemea na kutaka kuwaridhisha marafiki zake na kufuata mkumbo. Ili kuhimili stress za kipindi hiki, ndio watu hugundua vilevi, sigara, mitandao au mchumba ili kukubalika.

Ukiwauliza vijana wengi sasa kuhusu urafiki, wanasema marafiki wao wengi ni rafiki-jina. “Rafiki” ambaye labda hawajawahi hata kuonana. Huyu kijana akipata shida haendi kwa watu, bali anaona ni kawaida kugeukia mitandao kutatua shida yake.

Nisemacho ni hiki: Hakuna tatizo kwenye kubeti, kunywa pombe wala matumizi ya mitandao, tatizo ni kutokuwa na balance ya matumizi. Tatizo ni kutawaliwa na pombe, sigara na mitandao, mpaka kukosa muda wa kuwa pekee yako, kuwa na familia na marafiki halisi. Sikiliza: ukiwa na marafiki, wachache ndio vizuri. Urafiki wa kweli ni nadra na ni gharama. Wengi tunaodhani ni marafiki ni washikaji na wasindikizaji tu wa kupita. Chagua marafiki vizuri bila ulafi wala unafiki. Usaliti mbaya hadi ahera ni kuisaliti nafsi yako takatifu, yaani kujikufuru, kutokujisamehe, kujihukumu kwa makosa usiyoweza kuyarekebisha, kulazimisha matamanio yasiyowezekana, kusubiri wengine wakuletee furaha na kuishi bila kutumia vipawa vyako. Usijisaliti. Jikubali!

Ikitokea umeketi na umeiweka simu yako mezani, haijalishi kama umeigeuza juu au chini, hiyo inatuma ujumbe kwa wale ulionao kuwa wao sio muhimu kama hao unaongea nao kwenye simu. Mitandao ya kijamii bila nidhamu na weledi inaanza kugeuka kama madawa ya kulevya, hivyo kuleta uraibu mkubwa. Baada ya muda, taaratibu kama taarabu, uraibu unaharibu mahusiano na watu, utakugharimu muda na pesa ili kutibu afya yako.

Kitu ambacho kizazi hiki kinahitaji kujifunza ni NIDHAMU katika kila kitu, iwe ya kazi, mahusiano na ustahimilivu ambao sio sawa na uvumilivu. Kuna baadhi ya vitu muhimu maishani kama mapenzi, furaha ya kweli, kuridhika na kazi, kujiamini, stadi za maisha ni vitu vinavyochukua muda kupatikani. Achana na njia za mkato mnato. Maana mitandao inatufunza kupata/kutafuta vitu kwa namna ya haraka bila jasho (immediatism).

Bila nidhamu na ustahimilivu katika dunia ya leo, kunaleta ongezeko la matukio ya kujiua, sonona, matumizi ya vilevi na kuwa misukule fulani, bila kusudi la kuendelea kuishi. Na zaidi, ni kupunguza ufanisi na ubunifu kazini. Unamuuliza mtu vipi kazi yako, anajibu; “kawaida tu”. Au unamwuliza vipi mahusiano yako, anasema; “aah hivyo hivyo tunakomaa. Anaonesha kutoridhika na chochote hapo, ila basi tu atafanyaje. Hatuna budi kujenga uhusiano na watu wanaotuzunguka, kusalimiana, kusaidiana na kujenga roho ya kuaminiana.

Hivyo kuanzia leo, jipe malengo ndugu yangu. Usichaji simu mbele ya kitanda, unapozungumza na watu au upo chakulani, weka simu mbali. Enzi na wekeza katika ushirikiano kuliko kushindana na watu. Achana na roho ya ubinafsi na umimi. Mwisho; ukitaka kuishi kwa furaha na amani: kwanza punguza matarajio juu ya watu. Pili, wajibika kwa matatizo yako. Huwezi kuumizwa wala kuangushwa na mtu au kitu usicho na matarajio nacho.

Follow on Twitter @IsaacGaitano

--

--